‘MCHELE WA PLASTIKI’ BALAA UPYA!

‘MCHELE WA PLASTIKI’ BALAA UPYA!

495
0
SHARE

KWA siku kadhaa sasa tangu kuibuka kwa taharuki nchini juu ya uwepo wa mchele wa bandia almaarufu mchele wa plastiki huku mamlaka za serikali zikikanusha ishu hiyo, lakini kadiri siku zinavyosonga, jambo hilo limekuwa likiibua balaa upya. Mapema wiki hii, mwanamke mmoja aliyejukana kwa jina la Zuwena Mapunda, mkazi wa Kimara-Baruti jijini Dar alizua timbwili zito na la aina yake baada ya kudai kuuziwa mchele unaodaiwa kuwa ni wa plastiki.

 

Zuwena aliuziwa mchele huo na mfanyabishara aliyetajwa kwa jina moja la Kijagwa. Akizungumza na Amani mbele ya duka la nafaka la Kijagwa lililopo Kimara-Baruti, Dar huku kukiwa na umati uliotaka kuushuhudia mchele huo baada ya kuwepo kwa madai hayo kwa muda mrefu, Zuwena alisema kuwa, alinunua mchele huo kwenye duka hilo kwa ajili ya chakula cha familia.

 

Zuwena alisema kuwa, baada ya kuupika kwa muda mrefu bila kuiva ndipo alipouchunguza kwa kuufinyanga na kuudunda chini ambapo alishangaa kuona unadunda badala ya kutawanyiwa. Alisema kuwa, baada ya kuona hivyo, ndipo akakumbuka kuwa kuna habari zinazohusu mchele wa plastiki kwa hiyo huenda utakuwa ndiyo wenyewe.

 

“Mimi ni mteja wa muda mrefu katika duka hili. Siku mbili zilizopita, nilikuja kununua mchele hapa lakini cha ajabu, baada ya kuupika kwa saa nyingi haukuiva. “Katika kujiuliza ni kwa nini, ndipo nikakumbuka kuna mchele wa plastiki ambao una sifa zote kama huo. Ndipo nikaamua kurudi dukani na kuurudisha. Kwa bahati mbaya mfanyabiashara huyu, akawa analeta jeuri ndiyo maana watu wakajazana hapa,” alisema Zuwena.

 

MSIKIE SHUHUDA HUYU

 

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ambaye ni mkazi wa Kimara-Baruti aliyejitambulisha kwa jina la Khadija Khalidi  alisema kuwa, ni mara yake ya kwanza kuona chakula kilichopikwa kwa saa zaidi ya tatu kikiwa kibichi na kutoonesha dalili yoyote ya kuiva.

 

“Mimi ni mama ntilie wa hapa sokoni (Kimara-Baruti), ninapika sana wali, lakini wali uliopikwa na mchele unaodaiwa kuwa ni wa plastiki uliniacha hoi. “Wakati songombingo kati ya Zuwena na Kijagwa linatokea, nilikuwa ninafuatilia kwa karibu kutaka kujua ukweli wa jambo hili maana kila mtu anasema lake.

 

“Taarifa zinaonesha mchele unaodaiwa ni wa plastiki ulipikwa kwa zaidi ya saa tatu lakini bado ulikuwa mbichi hivyo hili limenishangaza sana,” alisema shuhuda huyo. Akizungumza na Amani kwa sharti la kutotajwa gazetini, ndugu wa karibu wa mfanyabiashara huyo ambaye wamekuwa wakifanyabiashara pamoja kwenye Soko la Kimara-Baruti alisema kuwa, anashangaa ndugu yake kutuhumiwa kuuza mchele wa bandia ilihali mchele huo waliununua Mbeya na ndiko wanakonunua miaka na miaka.

“Siku zote mchele tunaoununua sisi ni kutoka Mbeya. Hata huu unaodaiwa ni wa plastiki pia tumeununua hukohuko. Ndiyo maana ninashangaa ndugu yangu kudaiwa kuuza mchele wa plastiki. “Binafsi ninaamini mchele wetu ni mzuri na siyo wa bandia,” alijitetea ndugu huyo wa karibu wa Kijagwa.

 

AKAMATWA NA POLISI

 

Baada ya kuibuka kwa timbwili hilo huku habari zikisambaa kuwa mchele wa plastiki upo, baadhi ya watu waliwapigia simu polisi ambao walifika na kumchukua Kijagwa kwa ajili ya mahojiano na usalama wake kwani raia wenye hasira kali walitaka kufanya vitendo haramu vya kujichukulia sheria mkononi kwa kutaka kumshushia kipondo jamaa huyo.

 

Wakati wanaondoka na jamaa huyo baada ya kulifunga duka hilo, polisi walisema kuwa, wanakwenda kumhoji kwa kina juu ya mahali alipoupata mchele huo kwa kuwa pamoja na kusema kuwa ameununua mkoani Mbeya lakini hakuwa na dokyumenti zozote.

SAMPULI ZACHUKULIWA

Wakati hayo yakiendelea, naye Bwana Afya wa Kata ya KimaraBaluti, Khalfani Mwigeni alifika
sokoni hapo na kuchukua sampuli ya mchele unaodhaniwa kuwa ni wa plastiki kwa ajili ya kuupeleka kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo kabla ya kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi.

 

“Nimechukua sampuli ya mchele huu kwa ajili ya kuupeleka kwa Bwana Afya wa Wilaya ya Ubungo. Yeye ndiye ataupeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi na nadhani majibu ya uchunguzi yatafikishwa kwa waandishi wa habari na kwenye Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Baruti kwa ajili ya kuwatangazia wananchi wa eneo hili ambao kwa sasa wamekumbwa na taharuki,” alisema Khalifani.

MWENYEKITI WA MTAA

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Kimara-Baruti, Aloyce Kinyonga aliwaomba wananchi kuwa na subira kwa kuwa suala hilo lipo kwenye mamlaka husika na muda siyo mrefu majibu ya utata huo yatakuwa hadharani.

“Naomba wananchi wangu wawe na utulivu katika kipindi chote ambacho suala hili tata linatafutiwa ufumbuzi, nikiri kwamba jambo hili limeibua  taharuki kwa wakazi wengi wa mtaa wangu, lakini wasiwe na wasiwasi na chakula ambacho wamekuwa wakinunua katika masoko yetu kwa kuwa serikali ipo kwa ajili ya kuwalinda wananchi wake,” alisema Kinyonga.

 

KUHUSU MCHELE WA PLASTIKI

Mara baada ya kuibuka kwa taarifa za kuwepo kwa mchele wa plastiki nchini miezi kadhaa iliyopita, Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) ilikanusha vikali taarifa hizo. Hata hivyo, kwa mujibu wa wafanyabiashara wa nafaka jijini Dar, mchele unaosemekana ni wa plastiki siyo kwamba ni plastiki kama plastiki isipokuwa ni jina uliopewa mchele huo unaolimwa Mbeya unaoitwa ‘mchele wa plastiki kutoka Mbeya’.

DCI BOAZ ATOA ONYO

Kufuatia Watanzania kuwa na hofu juu ya mchele huo wakihofia afya zao, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz alitoa onyo kali kwa watumiaji wa mitandao ya jamii ambao wamekuwa wakisambaza video za upotoshaji juu ya kuwepo kwa mchele huo.

DCI Boaz aliliagiza Jeshi la Polisi kuanza mara moja kuwashughuliakia na kuwachukulia hatua za kisheria watu wenye tabia hiyo.

 

WAZIRI ATINGA ENEO LA TUKIO

Kufuatia sakata hilo la mchele unaodaiwa kuwa ni wa plastiki, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwaijage, alilazimika kufika eneo la tukio na kuzungumza na mmilikiwa wa duka.

“Ninachosema sitaki kuelekezwa kama unavyotaka kufanya, tumetuma wataalamu kwa lengo la kuupima huo mchele lakini umewakatalia, hujui ni kwa namna gani suala hili linatusumbua, hujui ni kwa namna gani leo sijalala kwa sababu ya suala hili, sasa nataka kwanza unipe leseni zote za uuzaji wa bidhaa za duka lako.

“Usiombe kupima kwa sasa, kwani mimi siyo mtaalamu, sasa kama ulikuwa tayari kufanya hivyo ulikuwa na sababu gani ya kuwakatalia wataalamu? Kwa sasa sitaki mazungumzo wala maelezo yoyote kutoka kwako, nipatie leseni na hatua zingine zitafuata,” alisema Mwijage.

NO COMMENTS